Tuesday, July 2, 2013

Mpango wa AGOA ulioiingizia Tanzania Sh92.8trilioni

Wafanyabiashara Tanzania watumia asilimia 8

Ukuzaji fursa za kiuchumi Afrika, (African Growth and Opportunity Act), AGOA, ni mpango mahsusi ulioanzishwa kwa ajili ya kuziwezesha nchi za Afrika kuuza bidhaa zao nchini Marekani.

Mpango huo upo kwa mujibu wa sheria baada ya kupitishwa Mei 18, 2000 na kwamba mpango huo unasaidia nchi za Afrika ikiwamo Tanzania kuuza bidhaa zao, kukuza mitaji pamoja na kupanua masoko kiuchumi.

Aliyekuwa Rais wa Marekani, George W. Bush alitia saini Mkataba wa Biashara kati ya Mataifa ya Afrika na Amerika, kupitia AGOA mwaka 2004.

Tanzania ambayo ni mmoja wa wanachama wa AGOA, ni miongoni mwa nchi zinazofaidika na mpango huo kwa kuuza bidhaa mbalimbali Marekani na kuingiza Sh92.8 trilioni hadi mwaka 2011, ikiwa ni zaidi ya asilimia 36.

Mwaka 2010, mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini Marekani yaliingiza Dola 15 milioni (Sh24 bilioni) ikiwa ni juu ya asilimia 73.1 tangu mwaka 2000.

Makubaliano ya biashara

 Mbali na mpango wa AGOA, Marekani ilisaini mkataba uitwao; Trade and Investment Framework Agreements (TIFA) na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2008, na Soko la Pamoja kwa Nchi za Kusini na Mashariki (Comesa) mwaka 2001. Tanzania ni mwanachama wa jumuiya zote hizo.

Marekani imekuwa ikijaribu mpango wake wa biashara na Afrika Mashariki na hata mwakilishi wake, katika masuala ya biashara Balozi, Ron Kirk aliwahi kuitembelea Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka huo, 2011 lengo ni kuimarisha uhusiano wa biashara kati ya Tanzania na Marekani.

Tanzania ni kati ya mataifa 136 yanayofanya biashara na Marekani na tangu kipindi hicho, jumla ya biashara za kuuza na kununua zinafikia Dola 316 milioni. Tanzania ni nchi ya 121 inayosafirisha kwa wingi bidhaa zake kwenda Marekani.

Kwa mwaka 2011, Marekani iliuza bidhaa zake Tanzania zenye thamani ya Dola 258 milioni, sawa na asilimia 57.7, ikiwa ni zaidi ya Dola 94 milioni tangu mwaka 2010, na zaidi ya asilimia 474.7 tangu  mwaka 2000.

Nchi hiyo pia imenunua kutoka Tanzania mashine mbalimbali za Dola 61 milioni, ngano (Dola 53 milioni), bidhaa za nguo (Dola25 milioni), mpira (Dola 15 milioni), na mashine za umeme za Dola 13 milioni.
Kwa mazao ya kilimo, Marekani ilinunua; kahawa, viungo, chai zilizoliingizia taifa Dola 29 milioni, madini (Dola 9 milioni, Knit Apparel Dola 5 milioni), mbogamboga ziliingiza Dola 5 milioni, matunda, korosho Dola 2 milioni na kahawa iliyoingiza Dola 28 milioni.

Kimsingi, Marekani na Tanzania ni washirika wakubwa katika biashara hasa katika Ukanda wa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara. Nchi hiyo iko katika harakati za kuwekeza kupitia mpango wake wa Millennium Challenge Account, Feed the Future na Partnership for Growth (PFG).

PFG, ni mpango wa kwanza wa Rais Barack Obama kwa ajili ya kukuza uchumi wa nchi zinazoendelea, demokrasia na utawala bora.

Nafasi za biashara

 Pamoja na kuwapo kwa nafasi za kuuza bidhaa mbalimbali nchini Marekani kupitia AGOA, wafanyabiashara wanatumia asilimia nane pungufu ya nafasi zinazotolewa na Marekani.

Kutokana na hali hiyo, Serikali inawataka wafanyabiashara kutumia nafasi hiyo kwa ajili ya kukuza kipato chao na cha taifa kwa kufanya biashara na taifa hilo lililostawi kiuchumi.

Akizungumza kwenye Mkutano wa mwaka wa TCCIA, Juni mwaka huu, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk  Abdallah Kigoda, anasema pamoja na kuwepo wigo mpana wa biashara kama; AGOA, Jumuiya ya Afrika Mashariki, (EAC), Umoja wa Ulaya (EU), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afika (Sadc), Tanzania inashiriki katika Jumuiya hizi katika nafasi ndogo.

 “Ni wakati wa wafanyabiashara kuzalisha mali kwa wingi na bora, kisha kuuza nje ikiwamo katika jumuiya mbalimbali zenye wigo mpana wa biashara,” anasema Dk Kigoda.

Dk Kigoda anasema, TCCIA lazima itoe elimu kwa wanachama wake, hasa kuhusu umuhimu wa uzalishaji na usindikaji mali ulio bora na kuuza nje ili kuongeza pato kwa mkulima kwa mazao bora.

Uwekezaji wa Marekani Tanzania

Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC, Raymond Mbilinyi anasema  uwekezaji wa taasisi za nje nchini, umekua kwa asilimia 10 na ulitarajiwa kuingiza Dola13 bilioni hadi kufikia mwishoni mwa 2012.

Hata hivyo, China inaonekana kuteka sehemu kubwa ya uwekezaji Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania ikilinganishwa na Marekani. Mpaka sasa, China imewekeza Dola1.4 bilioni ikiwa ni zaidi ya Marekani ambayo imewekeza Dola950 milioni Tanzania.

Ujio wa Rais Barack Obama  leo unaweza kuongeza wigo wa nchi yake kuwekeza Tanzania hasa kupitia mpango wa Millennium Challenge Corporation, MCC.

Akithibitisha hayo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe anasema uwekezaji utaongezeka kupitia mpango wa MCC, ambao utafadhili masuala ya elimu, afya na miradi ya barabara.

MCC, ni mpango ulioasisiwa na Baraza la Congress la Marekani mwaka 2004 kwa ajili ya kusaidia nchi zinazoendelea, na mwaka 2011 uliisaidia Tanzania Dola 698 milioni kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Tanzania imekuwa ikipata misaada ya MCC kwa elimu, miundombinu na afya...tutafanya mazungumzo kuhusu masuala ya kiuchumi, nishati Afrika na maendeleo ya uchumi na jinsi ya njia mbalimbali za uwekezaji.”

Mpango mwingine uliopo katika kukuza uchumi ni kupitia Millennium Challenge Account, MCA, ambao kazi yake ni kuendeleza sekta ya usafiri, umeme na maji.

No comments: