Thursday, June 13, 2013

CCM watumia udiwani kufanya kampeni za urais

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM na mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Abdallah Bulembo, wiki hii aligeuza kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata za Kaloleni, Elerai, Kimandolu na Themi, jijini Arusha kuwa za urais 2015 kwa kuwashambulia Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA na Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF.

Bulembo aliyekuwa akihutubia mkutano wa kampeni eneo la Stadium Bar kumnadi mgombea wa CCM Kata ya Kaloleni, alitumia muda mrefu kupiga propaganda za uchaguzi mkuu ujao badala ya kumnadi mgombea hali iliyowafanya wananchi wachache waliohudhuria mkutano huo kupaza sauti za kumtaka kutangaza sera badala ya kuzungumzia watu.

Kama vile hakusoma mazingira na nyuso za wasikilizaji wake ambao walionekana dhihiri kuchukizwa na hotuba yake, Bulembo aliwaomba Watanzania kutompigia kura za urais Dk. Slaa akidai atawaasi kama alivyoacha upadri na “kuoa mtawa, Rose Kamili.”

Kamili ni mzazi mwenzake Dk. Slaa, lakini hajawahi kuwa mtawa.

Kuhusu Profesa Lipumba, kada huyo wa CCM alidai asichaguliwe kwa sababu ni mzoefu wa kushindwa baada ya kuanza harakati za kuwania kiti cha urais tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 hadi sasa.

“Sifa ya maprofesa ni kufanya tafiti na kuandika vitabu vya kitaaluma. Sasa huyo Profesa Lipumba atakuja kuandika kitabu cha uzoefu wa kushindwa urais? Hafai huyu na kamwe Watanzania msimchague 2015. Mimi ni mjumbe wa CC na ninaahidi CCM tutawaletea mgombea safi,” alisema Bulembo na kuzua minong’ono miongoni mwa wasikilizaji.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo walisema kitendo cha Bulembo kuacha kumnadi mgombea na kugeukia kumshambulia Dk. Slaa ni dalili kuwa CCM inamhofia katibu huyo mkuu wa CHADEMA katika uchaguzi mkuu ujao 2015.

Dk. Slaa hajatangaza kugombea urais, lakini mvuto wake na upinzani mkubwa aliouonyesha dhidi ya Rais Jakaya Kikwete katika uchaguzi uliopita bado unaitia kiwewe CCM, hasa iwapo uchaguzi huo utafanyika kwa kutumia katiba mpya itakayounda tume huru ya uchaguzi tofauti na ya sasa inayodaiwa kukipendelea chama hicho tawala.

Katika uchaguzi uliopita, Dk. Slaa alipata zaidi ya kura milioni mbili nyuma ya Rais Kikwete ingawa kulikuwapo tuhuma za uchakachuaji na ushiriki wa vyombo vya dola kuibeba CCM na wagombea wake.

No comments: