Thursday, June 13, 2013

Mzozo wa ving’amuzi watua bungeni

SERIKALI imetakiwa kuruhusu matumizi ya teknolojia ya analojia sambamba na dijitali hadi hapo nchi itakapokuwa tayari kuendana na mabadiliko hayo ya kiteknolojia.

Mapendekezo hayo yalitolewa bungeni jana na Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali wakati akiwasilisha maelezo binafsi kuhusu matumizi sambamba kati ya teknolojia ya dijitali na analojia.
Machali alisema kuwa utaratibu wa kuzima mitambo ya analojia kwa mikoa mingine usitishwe hadi hapo vituo vya luninga vitakapokuwa na uwezo wa kurusha matangazo yao moja kwa moja kwa kutumia teknolojia hiyo ya dijitali.

“Serikali izingatie hali ya kipato cha matumizi bila kujali matakwa ya kiteknolojia au ya kibiashara. Utu wa Mtanzania ni vyema ukatazamwa kwa jicho la utaifa zaidi,” alisema.

Machali alisema kuwa serikali ina jukumu la kuhakikisha wananchi wote waliokuwa wanapata matangazo ya luninga kwa njia ya analojia wanapata sambamba kwa njia ya dijitali. Alisema kuwa ili kupata matangazo hayo ya dijitali, mwananchi anahitaji kisimbuzi (king’amuzi), kwamba visimbuzi viko vya aina mbili; DVB-T na DVB-T2.

“Kisimbuzi cha DVB-T2 kinaweza kupokea matangazo kutoka kwenye mitambo ya DVB-T2 na DVB-T. Kisimbuzi cha DVB-T kinaweza kupokea matangazo kutoka kwenye mitambo ya DVB-T peke yake,” alisema. Machali alisema kuwa tatizo la kuhamia katika teknolojia ya dijitali ni kubwa kwa wamiliki wa vituo vya luninga na kwa wananchi wa kawaida. Kwamba maamuzi ya kuhamia kwenye teknolojia hiyo yamefanywa kwa haraka sana.

Alisema kuwa bila kufanya utafiti, kwa kulinganisha tu idadi ya mitambo ya analojia iliyokuwepo na ya dijitali iliyopo, ukweli huo unajidhihirisha kwenye mikoa mfano Dodoma kulikuwa na mitambo sita ya analojia; ITV, EATV, TBC, Star tv, Channel 10 na Agape.

Kwamba sasa hivi kuna mitambo miwili tu ya dijitali ya Star Media na Agape Associates wakati Mwanza kulikuwa na mitambo sita ya analojia; ITV, EATV, TBC, Star tv, Channel 10 na Agape TV lakini sasa ipo miwili ya Star Media na Agape Associates.

No comments: