Friday, June 28, 2013

Mandela ni simanzi

NI simanzi kila kona ya dunia! Baba wa Taifa la Afrika Kusini na kipenzi cha Waafrika kwa jumla, Nelson Rolihlahla Madiba Mandela (94), ameibua simanzi baada ya familia yake kukutana kwenye eneo la makaburi ya ukoo kwa ajili ya kuandaa mazishi ya rais huyo wa kwanza mweusi wa nchi hiyo. 



 Hayo yanakuja kufuatia afya ya mzee huyo kuwa tete akisumbuliwa na maradhi ya mapafu ambapo leo anatimiza siku 20 tangu alipokimbizwa katika Hospitali ya Mediclinic Heart iliyopo jijini Pretoria, Afrika Kusini ‘Sauzi’.
 

Historia ya matatizo ya mapafu ya Mzee Madiba ilianza alipokuwa kwenye Gereza la Kisiwa cha Robben karibu na Cape Town kwa miaka 27 ambapo aliachiwa huru mwaka 1990 na akaendelea kutumikia nchi kama rais wa kwanza wa Afrika Kusini huru kuanzia mwaka 1994 hadi 1999.

Habari zilieleza kuwa kabla ya kwenda katika makaburi hayo ya ukoo yaliyopo katika Kijiji cha Qunu jimboni Eastern Cape kwenye makazi ya Mzee Madiba, familia nzima ilikutana kwa ajili ya kikao cha siri lakini haikujulikana mara moja walichokijadili.
 
WAANDISHI WAPIGANA VIKUMBO
Hata hivyo, waandishi wa Sauzi na vyombo vya kimataifa kama vile BBC, CNN, Sky News na wengine wengi ambao tayari wamejazana kijijini hapo, walizuiwa mita chache getini kwani hawakutakiwa kujua kilichokuwa kinajadiliwa na familia.

Kuhusu safari ya makaburini ilielezwa kuwa ni mila za watu wa Kabila la Xhosa ambapo wanaukoo hulazimika kwenda kwenye makaburi kufanya tambiko wanapohisi kuna mtu wa ukoo huo ataaga dunia muda mfupi mbele.

“Mzee Madiba alishaonesha mahali atakapozikwa, ni kwenye makaburi ya ukoo wa Madiba walipozikwa ndugu zake wengine ndiyo maana walikwenda kupafanyia ‘mambo’,” uliandika mtandao mmoja wa Sauzi.
Kwa upande wake mkewe, Graca Machel alilazimika kuahirisha safari yake ya kikazi ili kuwa karibu naye huku mkewe wa zamani ambaye walitalikiana mwaka 1996, Winnie Madikizela Mandela akiwa miongoni mwa wanafamilia waliojumuika kushirikiana katika maandalizi hayo.
 
HALI YA KIJIJI CHA QUNU
Habari zinasema kuwa Kijiji cha Qunu kimetawaliwa na vilio na simanzi kubwa zinazoongozwa na ukoo wa Madiba kama ilivyo dunia nzima ambapo macho na masikio ya wengi yameelekezwa nchini humo.
 
 MAANDALIZI MAKUBWA
Tayari kumekuwa na maandalizi makubwa ya kumpumzisha kiongozi huyo huku wageni wakiendelea kumiminika Sauzi kwa kuamini si wa kupona tena.
 
BARABARA KIWANGO CHA LAMI
Habari zilizidi kueleza kuwa tayari kuna matengenezo ya barabara kwa kiwango cha lami kutoka Eastern Cape hadi kijijini hapo huku greda likionekana kwenye uwanja mkubwa uliopo kwenye makazi ya Mzee Madiba.
 
UWANJA WA NDEGE
Pia kuna matengenezo makubwa ya Uwanja wa Eastern Cape ambao umefikia kwenye kiwango cha kutua ndege kubwa aina ya Boeing 737 kwa ajili ya wageni watakaokwenda kijijini Qunu.
 
UJIO WA OBAMA
Kwa mujibu wa sosi wetu Sauzi, ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama umeingia shubiri nchini humo kwa vile habari ya mjini ni Mzee Madiba hivyo shamrashamra za kumpokea rais huyo hazina nguvu  ‘automatiki’.
Kuhusu hilo, imeelezwa kuwa Obama hataruhusiwa kwenda kumuona Madiba jambo lililoibua maswali kuwa iweje rais mkubwa kama huyo asiende kumjulia hali kiongozi huyo mkubwa duniani.
 
HISTORIA
Mzee Madiba alizaliwa Julai 18, 1918 katika kijiji kidogo cha Mvezo kilichoko katika Wilaya ya Umtata Jimbo la Eastern Cape nchini humo.
Jina lake lingine la katikati la Rolihlahla linamaanisha ‘kuvuta tawi la mti’ au ‘mleta matatizo’ huku Madiba likiwa jina lake la utotoni.
 
HARAKATI
Baada ya ushindi katika uchaguzi wa mwaka 1948 wa Chama cha Kiafrikana cha National Party (NP), ambacho kiliunga mkono sera za utengano wa  kibaguzi, Mzee Madiba alianza kushiriki harakati za kisiasa.
Mzee Madiba aliongoza kampeni maarufu ya uasi ya Chama cha ANC mwaka 1952 na 1955 katika harakati za kupigania ukombozi wa mtu mweusi.

Katika kipindi hicho, Madiba na mwanasheria mwenzake na rafiki yake mkubwa, Oliver Tambo, waliendesha Kampuni ya Sheria ya Mandela na Tambo, wakitoa ushauri wa kisheria bure au kwa gharama ndogo kwa wazalendo weusi waliokosa uwakilishi wa kisheria.
 
UBAGUZI
Mwaka 1961, Madiba alikuwa kiongozi wa Kundi la Kijeshi la ANC, Umkhonto we Sizwe ambalo tafsiri yake ni ‘Mkuki wa Taifa’ ambalo pia lilipewa ufupisho wa MK na alishiriki kuliunda na mwenzake mwingine.
Aliendesha kampeni za hujuma dhidi ya jeshi na maeneo ya serikali na kufanya mipango ya kuwezesha vita ya msituni iwapo hujuma zitashindwa kumaliza ubaguzi wa rangi.
 
KUKAMATWA
Agosti 5, mwaka 1962, Madiba alikamatwa baada ya kuishi akizikimbia mamlaka husika kwa miezi 17 na akafungwa katika ngome ya Johannesburg Fort huko Sauzi.

Kukamatwa kwake kunadaiwa kufanikishwa na makachero wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA), waliozigusia mamlaka za usalama Afrika Kusini aliko Mandela.

Siku tatu baadaye, mashitaka ya kuendesha mgomo na kuondoka nchini isivyo halali mwaka 1961 yakasomwa mahakamani, Oktoba 25, 1962 alifungwa jela miaka mitano.
 
GEREZANI
Baada ya kutiwa hatiani kwa kesi ya uhaini, Juni 12, 1964, Mahakama ilitoa adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa Madiba na wenzake.

Madiba alifungwa jela katika Gereza la Kisiwa cha Robben ambako alikaa kwa kipindi cha miaka 27.
Wakati akiwa jela, umaarufu wake uliongezeka na kujulikana kama kiongozi muhimu kabisa wa wazalendo weusi Afrika Kusini.

KUACHIWA
Februari 2, 1990, kaburu Rais Frederik Willem de Klerk alibatilisha amri inayoipiga marufuku ANC na taasisi nyingine zilizopinga ubaguzi wa rangi na akatangaza kwamba Madiba ataachiwa kutoka jela muda si mrefu.
Mandela aliachiwa kutoka gerezani Februari 11, 1990, tukio hilo lilitangazwa duniani kote.
 
AFRIKA KUSINI MPYA
Baada ya shujaa Madiba kuachiwa, majadiliano ya kumaliza ubaguzi wa rangi nchini humo  yakafuata.
Madiba alirudi katika uongozi wa Chama cha African National Congress (ANC) kati ya mwaka 1990 na 1994.

Uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi wa Afrika Kusini isiyo ya kibaguzi ulifanyika Aprili 27, 1994 ambapo ANC ilishinda kwa asilimia 62 na Madiba kama kiongozi wa ANC aliapishwa Mei 10, 1994 kuwa rais wa kwanza mweusi.
 
NDOA
Mandela alioa mara tatu na kujaliwa watoto sita, wajukuu 20 na idadi kubwa ya vitukuu.
 
NDOA YA KWANZA
Ndoa ya kwanza ya Madiba alifunga na Evelyn Ntoko Mase ambaye alizaa naye watoto wawili.
Wawili hao waliachana mwaka 1957, walitalikiana baada ya harakati zake za ukombozi huku mkewe akiwa Shahidi wa Yehova, dini ambayo ilihitaji kutosimama upande wowote kisiasa.
 
NDOA YA PILI
Ndoa ya pili ya Madiba ilikuwa na Winnie Mandela ambaye alionana naye Johannesburg akiwa mfanyakazi wa kwanza mweusi wa jiji.

Madiba na Winnie walijaliwa mabinti wawili, Zenani (Zeni), aliyezaliwa mwaka 1958 na Zindziswa (Zindzi) Mandela-Hlongwane, aliyezaliwa 1960.

Wakati mume wake akitumikia kifungo cha maisha, baba wa Winnie alikuwa Waziri wa Kilimo katika Jimbo la Transkei. Ndoa yao ilivunjika Aprili 1992 na talaka kufikiwa Machi 1996, ikichangiwa na mtengano mrefu wa kisiasa.
 
NDOA YA TATU
Madiba alioa tena katika kumbukumbu yake ya siku ya kuzaliwa ya kutimiza miaka 80 ya mwaka 1998.
Wakati huu alimuoa Graca Simbine Machel, mjane wa aliyekuwa Rais wa Msumbiji, marehemu Samora Machel na mshirika wa ANC ambaye alikufa katika ajali ya ndege mwaka 1986.
 
MARADHI
Madiba alikuwa rais mkubwa kabisa kuchaguliwa Afrika Kusini wakati alipoingia madarakani akiwa na umri wa miaka 75 mwaka 1994, alidhamiria kutowania muhula wa pili na alistaafu mwaka 1999, akirithiwa na Thabo Mbeki.

Julai 2001, Madiba aligundulika kuwa na saratani ya kibofu ambapo alitibiwa kwa mionzi kwa kipindi cha wiki saba.

Mwaka 2003, kifo cha Madiba kilitangazwa kimakosa na Shirika la Habari la Marekani (CNN).
Mwaka 2007, kundi la mrengo wa kulia lilisambaza barua pepe bandia na ujumbe wa simu za mikononi kuwa mamlaka zimeficha kifo cha Madiba na kwamba weupe nchini humo watauawa baada ya mazishi yake.

Wakati hayo yakitokea, Madiba alikuwa mapumzikoni nyumbani kwa mkewe Msumbiji.
Juni 2004, akiwa na umri wa miaka 85, Madiba alitangaza kuwa anajiuzulu katika shughuli za kijamii.
Siku ya kutimiza miaka 90 ya kuzaliwa ya Madiba ilisherehekewa nchini kote Julai 18, mwaka 2008, huku sherehe kubwa ikifanyika kijijini kwake Qunu.

Pamoja na kutojionesha sana wakati wa michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika nchini humo mwaka 2010, Madiba alionekana wakati wa sherehe za ufunguzi.

Januari 2011, alilazwa katika hospitali binafsi ya Millpark, jijini Johannesburg kwa kile kilichoelezwa kipindi hicho na taasisi yake kuwa uchunguzi wa kawaida na kuibua minong’ono mizito katika vyombo vya habari kuhusu kuzidi kuzorota kwa afya yake kabla ya hivi karibuni hali kuwa mbaya akisumbuliwa na mapafu.

No comments: