NI
simanzi kila kona ya dunia! Baba wa Taifa la Afrika Kusini na kipenzi
cha Waafrika kwa jumla, Nelson Rolihlahla Madiba Mandela (94), ameibua
simanzi baada ya familia yake kukutana kwenye eneo la makaburi ya ukoo
kwa ajili ya kuandaa mazishi ya rais huyo wa kwanza mweusi wa nchi hiyo.
Hayo
yanakuja kufuatia afya ya mzee huyo kuwa tete akisumbuliwa na maradhi
ya mapafu ambapo leo anatimiza siku 20 tangu alipokimbizwa katika
Hospitali ya Mediclinic Heart iliyopo jijini Pretoria, Afrika Kusini
‘Sauzi’.
Historia ya matatizo ya mapafu ya Mzee Madiba ilianza
alipokuwa kwenye Gereza la Kisiwa cha Robben karibu na Cape Town kwa
miaka 27 ambapo aliachiwa huru mwaka 1990 na akaendelea kutumikia nchi
kama rais wa kwanza wa Afrika Kusini huru kuanzia mwaka 1994 hadi 1999.
Habari
zilieleza kuwa kabla ya kwenda katika makaburi hayo ya ukoo yaliyopo
katika Kijiji cha Qunu jimboni Eastern Cape kwenye makazi ya Mzee
Madiba, familia nzima ilikutana kwa ajili ya kikao cha siri lakini
haikujulikana mara moja walichokijadili.
WAANDISHI WAPIGANA VIKUMBO
Hata
hivyo, waandishi wa Sauzi na vyombo vya kimataifa kama vile BBC, CNN,
Sky News na wengine wengi ambao tayari wamejazana kijijini hapo,
walizuiwa mita chache getini kwani hawakutakiwa kujua kilichokuwa
kinajadiliwa na familia.
Kuhusu safari ya makaburini ilielezwa kuwa
ni mila za watu wa Kabila la Xhosa ambapo wanaukoo hulazimika kwenda
kwenye makaburi kufanya tambiko wanapohisi kuna mtu wa ukoo huo ataaga
dunia muda mfupi mbele.
“Mzee Madiba alishaonesha mahali
atakapozikwa, ni kwenye makaburi ya ukoo wa Madiba walipozikwa ndugu
zake wengine ndiyo maana walikwenda kupafanyia ‘mambo’,” uliandika
mtandao mmoja wa Sauzi.
Kwa upande wake mkewe, Graca Machel
alilazimika kuahirisha safari yake ya kikazi ili kuwa karibu naye huku
mkewe wa zamani ambaye walitalikiana mwaka 1996, Winnie Madikizela
Mandela akiwa miongoni mwa wanafamilia waliojumuika kushirikiana katika
maandalizi hayo.
HALI YA KIJIJI CHA QUNU
Habari zinasema kuwa
Kijiji cha Qunu kimetawaliwa na vilio na simanzi kubwa zinazoongozwa na
ukoo wa Madiba kama ilivyo dunia nzima ambapo macho na masikio ya wengi
yameelekezwa nchini humo.
MAANDALIZI MAKUBWA
Tayari
kumekuwa na maandalizi makubwa ya kumpumzisha kiongozi huyo huku wageni
wakiendelea kumiminika Sauzi kwa kuamini si wa kupona tena.
BARABARA KIWANGO CHA LAMI
Habari
zilizidi kueleza kuwa tayari kuna matengenezo ya barabara kwa kiwango
cha lami kutoka Eastern Cape hadi kijijini hapo huku greda likionekana
kwenye uwanja mkubwa uliopo kwenye makazi ya Mzee Madiba.
UWANJA WA NDEGE
Pia
kuna matengenezo makubwa ya Uwanja wa Eastern Cape ambao umefikia
kwenye kiwango cha kutua ndege kubwa aina ya Boeing 737 kwa ajili ya
wageni watakaokwenda kijijini Qunu.
UJIO WA OBAMA
Kwa mujibu
wa sosi wetu Sauzi, ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama umeingia
shubiri nchini humo kwa vile habari ya mjini ni Mzee Madiba hivyo
shamrashamra za kumpokea rais huyo hazina nguvu ‘automatiki’.
Kuhusu
hilo, imeelezwa kuwa Obama hataruhusiwa kwenda kumuona Madiba jambo
lililoibua maswali kuwa iweje rais mkubwa kama huyo asiende kumjulia
hali kiongozi huyo mkubwa duniani.
HISTORIA
Mzee
Madiba alizaliwa Julai 18, 1918 katika kijiji kidogo cha Mvezo
kilichoko katika Wilaya ya Umtata Jimbo la Eastern Cape nchini humo.
Jina
lake lingine la katikati la Rolihlahla linamaanisha ‘kuvuta tawi la
mti’ au ‘mleta matatizo’ huku Madiba likiwa jina lake la utotoni.
HARAKATI
Baada
ya ushindi katika uchaguzi wa mwaka 1948 wa Chama cha Kiafrikana cha
National Party (NP), ambacho kiliunga mkono sera za utengano wa
kibaguzi, Mzee Madiba alianza kushiriki harakati za kisiasa.
Mzee
Madiba aliongoza kampeni maarufu ya uasi ya Chama cha ANC mwaka 1952 na
1955 katika harakati za kupigania ukombozi wa mtu mweusi.
Katika
kipindi hicho, Madiba na mwanasheria mwenzake na rafiki yake mkubwa,
Oliver Tambo, waliendesha Kampuni ya Sheria ya Mandela na Tambo, wakitoa
ushauri wa kisheria bure au kwa gharama ndogo kwa wazalendo weusi
waliokosa uwakilishi wa kisheria.
UBAGUZI
Mwaka 1961, Madiba
alikuwa kiongozi wa Kundi la Kijeshi la ANC, Umkhonto we Sizwe ambalo
tafsiri yake ni ‘Mkuki wa Taifa’ ambalo pia lilipewa ufupisho wa MK na
alishiriki kuliunda na mwenzake mwingine.
Aliendesha kampeni za
hujuma dhidi ya jeshi na maeneo ya serikali na kufanya mipango ya
kuwezesha vita ya msituni iwapo hujuma zitashindwa kumaliza ubaguzi wa
rangi.
KUKAMATWA
Agosti 5, mwaka 1962, Madiba alikamatwa baada
ya kuishi akizikimbia mamlaka husika kwa miezi 17 na akafungwa katika
ngome ya Johannesburg Fort huko Sauzi.
Kukamatwa kwake kunadaiwa
kufanikishwa na makachero wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA),
waliozigusia mamlaka za usalama Afrika Kusini aliko Mandela.
Siku
tatu baadaye, mashitaka ya kuendesha mgomo na kuondoka nchini isivyo
halali mwaka 1961 yakasomwa mahakamani, Oktoba 25, 1962 alifungwa jela
miaka mitano.
GEREZANI
Baada ya kutiwa hatiani kwa kesi ya
uhaini, Juni 12, 1964, Mahakama ilitoa adhabu ya kifungo cha maisha jela
kwa Madiba na wenzake.
Madiba alifungwa jela katika Gereza la Kisiwa cha Robben ambako alikaa kwa kipindi cha miaka 27.
Wakati akiwa jela, umaarufu wake uliongezeka na kujulikana kama kiongozi muhimu kabisa wa wazalendo weusi Afrika Kusini.
KUACHIWA
Februari
2, 1990, kaburu Rais Frederik Willem de Klerk alibatilisha amri
inayoipiga marufuku ANC na taasisi nyingine zilizopinga ubaguzi wa rangi
na akatangaza kwamba Madiba ataachiwa kutoka jela muda si mrefu.
Mandela aliachiwa kutoka gerezani Februari 11, 1990, tukio hilo lilitangazwa duniani kote.
AFRIKA KUSINI MPYA
Baada ya shujaa Madiba kuachiwa, majadiliano ya kumaliza ubaguzi wa rangi nchini humo yakafuata.
Madiba alirudi katika uongozi wa Chama cha African National Congress (ANC) kati ya mwaka 1990 na 1994.
Uchaguzi
wa kwanza wa vyama vingi wa Afrika Kusini isiyo ya kibaguzi ulifanyika
Aprili 27, 1994 ambapo ANC ilishinda kwa asilimia 62 na Madiba kama
kiongozi wa ANC aliapishwa Mei 10, 1994 kuwa rais wa kwanza mweusi.
NDOA
Mandela alioa mara tatu na kujaliwa watoto sita, wajukuu 20 na idadi kubwa ya vitukuu.
NDOA YA KWANZA
Ndoa ya kwanza ya Madiba alifunga na Evelyn Ntoko Mase ambaye alizaa naye watoto wawili.
Wawili
hao waliachana mwaka 1957, walitalikiana baada ya harakati zake za
ukombozi huku mkewe akiwa Shahidi wa Yehova, dini ambayo ilihitaji
kutosimama upande wowote kisiasa.
NDOA YA PILI
Ndoa ya pili ya Madiba ilikuwa na Winnie Mandela ambaye alionana naye Johannesburg akiwa mfanyakazi wa kwanza mweusi wa jiji.
Madiba
na Winnie walijaliwa mabinti wawili, Zenani (Zeni), aliyezaliwa mwaka
1958 na Zindziswa (Zindzi) Mandela-Hlongwane, aliyezaliwa 1960.
Wakati mume wake akitumikia kifungo cha maisha, baba wa Winnie alikuwa Waziri wa Kilimo katika Jimbo la Transkei. Ndoa yao ilivunjika Aprili 1992 na talaka kufikiwa Machi 1996, ikichangiwa na mtengano mrefu wa kisiasa.
NDOA YA TATU
Madiba alioa tena katika kumbukumbu yake ya siku ya kuzaliwa ya kutimiza miaka 80 ya mwaka 1998.
Wakati
huu alimuoa Graca Simbine Machel, mjane wa aliyekuwa Rais wa Msumbiji,
marehemu Samora Machel na mshirika wa ANC ambaye alikufa katika ajali ya
ndege mwaka 1986.
MARADHI
Madiba alikuwa rais mkubwa kabisa
kuchaguliwa Afrika Kusini wakati alipoingia madarakani akiwa na umri wa
miaka 75 mwaka 1994, alidhamiria kutowania muhula wa pili na alistaafu
mwaka 1999, akirithiwa na Thabo Mbeki.
Julai 2001, Madiba aligundulika kuwa na saratani ya kibofu ambapo alitibiwa kwa mionzi kwa kipindi cha wiki saba.
Mwaka 2003, kifo cha Madiba kilitangazwa kimakosa na Shirika la Habari la Marekani (CNN).
Mwaka
2007, kundi la mrengo wa kulia lilisambaza barua pepe bandia na ujumbe
wa simu za mikononi kuwa mamlaka zimeficha kifo cha Madiba na kwamba
weupe nchini humo watauawa baada ya mazishi yake.
Wakati hayo yakitokea, Madiba alikuwa mapumzikoni nyumbani kwa mkewe Msumbiji.
Juni 2004, akiwa na umri wa miaka 85, Madiba alitangaza kuwa anajiuzulu katika shughuli za kijamii.
Siku
ya kutimiza miaka 90 ya kuzaliwa ya Madiba ilisherehekewa nchini kote
Julai 18, mwaka 2008, huku sherehe kubwa ikifanyika kijijini kwake Qunu.
Pamoja
na kutojionesha sana wakati wa michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika
nchini humo mwaka 2010, Madiba alionekana wakati wa sherehe za ufunguzi.
Januari
2011, alilazwa katika hospitali binafsi ya Millpark, jijini
Johannesburg kwa kile kilichoelezwa kipindi hicho na taasisi yake kuwa
uchunguzi wa kawaida na kuibua minong’ono mizito katika vyombo vya
habari kuhusu kuzidi kuzorota kwa afya yake kabla ya hivi karibuni hali
kuwa mbaya akisumbuliwa na mapafu.